Rais Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuundwa kwa chombo maalumu cha upelelezi kitakachoshughulikia masuala yaliyoainishwa katika ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ikiwemo uchunguzi wa wahusika wa matukio ya uhalifu.
Rais Samia amesema chombo hicho kitafanya kazi ya kubaini watu waliohusika kupanga, kuratibu na kufadhili matukio hayo ya uvunjifu wa amani.
Amezungumza hayo leo Aprili 23, 2026, wakati akipokea ripoti ya Tume hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam, akisema chombo hicho kitaangalia kwa undani pia masuala ya madai ya watoto kutumika katika matukio hayo na hoja zinazohusu kutopatikana kwa baadhi ya miili.
Ameongeza kuwa chombo hicho kitashughulikia pia madai ya watu waliodaiwa kutekwa na taarifa zao kutopatikana pamoja na walioathirika nje ya maeneo ya vurugu.


