Serikali yasitisha ununuzi wa mahindi Songea

HomeKitaifa

Serikali yasitisha ununuzi wa mahindi Songea

Serikali imesitisha ununuzi mahindi katika Kituo Kikuu cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea kilichopo Ruhuwiko mkoani Ruvuma baada ya kubaini na kujiridhisha kuwa, mahindi mengi yanayopelekwa kwenye kituo hicho ni ya wafanyabiashara na si ya wakulima.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Wilbert Ibuge alitangaza uamuzi huo akiwa na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ambao walifika kituoni hapo kukagua kazi ya kununua mahindi inayofanywa na NFRA Kanda ya Songea katika wilaya za Songea na Mbinga.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 50 ambazo zinatumika kununua mahindi kutoka kwa wakulima ili kuwanusuru na kudodora kwa bei ya zao hilo.

Mkenda alisema mahindi hayo yatanunuliwa kupitia Vyama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) au vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa na kwa wakulima wadogo kwa magunia yasiyozidi 300 au tani 30 kwa kuwa wanataka rekodi ya kila mkulima aliyelima mahindi yanunuliwe na fedha zilizotolewa na Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa.

“Tutakagua hivyo wananchi au wakulima mkiona dalili za ukiukwaji wa ununuzi wa mahindi toeni taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo kwenye maeneo yenu,” alibainisha Mkenda.

error: Content is protected !!