Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje CHADEMA, John Mrema amesema hatua inayofuata kufuatia kuondolewa uanachama kwa wanachama wake 19 ni kumpatia taarifa hiyo Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson.
Uamuzi wa kuwafukuza uanachama Halima Mdee na wenzie 18, umefikiwa na Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) usiku wa kuamkia leo ambapo wamefutilia mbali rufaa waliokata wanachama hao 19 baada ya kuvuliwa uanacham na Kamati Kuu ya chama hicho.
“Katibu Mkuu [John Mnyika] ataandika barua rasmi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumjulisha uamuzi huu wa Baraza Kuu, kahiyo suala hili sasa litakuwa mikononi mwa spika. Baada ya hapo litakuwa limetoka mikononi mwa chama kwasababuhawana tena nafasi ya kukata rufaa mamlaka ya rufaa yao ilikuwa mwisho ni Baraza Kuu,” ameeleza Mrema.
Akizungumzia kuhusu sakata hilo, Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee amesema, “Nakwepa kuzungumza maneno makali kwasababu naheshimu viongozi wangu lakini sikujua CHADEMA umeanza kufanyika uhuni kwa kiwango hicho. Nitaongea siku nyingine lakini kilichofanyika pale hata Mbowe anajua ni uhuni.”
Zaidi ya kura 97% zilizopigwa zimekubaliana na suala la kuavua uanachama wanachama hao.