Tanzania, DRC kuinua uchumi kwa pamoja

HomeKitaifa

Tanzania, DRC kuinua uchumi kwa pamoja

Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekubaliana kushirikiana kujenga miundombinu ya reli ya kisasa na barabara ili kuimarisha biashara baina yao.

Hayo yamesemwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam katika mazungumzo baina ya Rais Samia Suluhu na Rais wa DRC ,Felix Tshisekedi aliyekuja nchini kwenye ziara ya kikazi ya siku nne.

Akizungumzia mambo waliyoyajadili na mgeni wake, Rais Samia Suluhu alisema wamekubaliana kujenga miundombinu ya barabara na reli zitakazounganisha mataifa hayo na kurahisisha biashara na uwekezaji.

Alisema mawaziri wa fedha wa DRC na Tanzania walikutana na kukubaliana kukopa Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa (SGR) kuanzia Kigoma hadi DRC.

Pia, alisema wamekubaliana kujenga barabara ya ushoroba wa kati itakayoiunganisha Tanzania na DRC ili kuimarisha biashara.

“Nimemhakikishia kwamba tuko tayari kufanya naye kazi ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo,” alisema Rais Samia na kusisitiza kwamba nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi.

Kuhusu usafiri wa anga, Rais Samia alisema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linafanya safari zake DRC, hata hivyo amemwomba Rais Tshisekedi ndege zake zitue katika miji mingine mikubwa ya Congo jambo ambalo amelikubali hivyo wanasubiri vibali tu.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alisema jambo kubwa walilojadili ni kuhusu usalama kwa sababu biashara na uwekezaji hautofanyika kusipokuwa na amani ya uhakika.

Alisema kwa bahati mbaya uchafuzi kwa kisiasa nchi kwake unafanywa na jirani yao ndiyo amana ameweka nguvu kushirikiana na majirani wengine hasa katika kujenga miundombinu.

“Suala la mawasiliano ni muhimu kuendelezwa kwa sababu yatatengeneza ajira kwa watu,” alisema Rais Tshisekdi na kuongeza kwamba wapo tayari kushirikiana na Tanzania.

Jana, viongozi hao walishuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mawasiliano na Posta.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wakati wakishuhudia uwekaji saini Mkataba wa makubaliano baina ya Tanzania na DRC, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2022. Kwa upande wa Tanzania, Mkataba huo ulisainiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye na kwa upande wa DRC uliwekwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Christophe Lutundula.

error: Content is protected !!