TMDA: Marufuku sigara hadharani

HomeKitaifa

TMDA: Marufuku sigara hadharani

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema ni kosa kisheria kuvuta sigara hadharani au kwenye maeneo ya mikusanyiko na atakayebainika kufanya hivyo atatozwa faini ya Tsh. 200,000 au kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita jela.

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TMDA, Gloria Matemu aliyasema hayo Aprili 9, 2022 katika Soko Kuu la Kariakoo, wakati wa kampeni ya kutoa elimu katika maeneo ya mikusanyo kuhusu madhara ya kutumia tumbaku na adhabu zake.

Alisema TMDA imepewa jukumu la kudhibiti matumizi ya tumbaku kwa lengo la kutoa elimu kuhusu matakwa ya sheria namba 121 kuanzia Aprili 30, 2022.

“Ukibainika unavuta tumbaku hadharani au katika mikusanyiko utatozwa faini ya Sh 200,000 au kutumikia adhabu ya miezi sita jela,” alisema.

Hivyo, aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe na masoko kutenga maeneo maalum ya kuvutia sigara kwa sababu watu wengi wanaathirika kutokana na watu wachache wanaovuta sigara.

Matemu alisema TMDA imefanya kampeni ya siku tano ya kutembelea kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama vituo vya mabasi na masoko, ili kuwaelimisha kuhusu madhara na namna sheria inavyofanya kazi.

Alisema kampeni hiyo imesaidia kufikisha elimu kwa wakazi wa Manispaa ya llala na lengo kuu ni kuwafikia Watanzania wote wafahamu kuhusu jukumu hilo la TMDA katika kudhibiti matumizi ya tumbaku ili kupunguza madhara yatokanayo na uvutaji huo.

Mkaguzi wa TMDA, Kanda ya Mashariki, Jafari Tolo alisema takwa la sheria ni kuzuia uvutaji wa sigara kwenye mikusanyiko ya watu na wamiliki wa maeneo yanayokusanya maeneo maalum ya wanaovuta kuvuta bila kuathiri wasiovuta.

Alisema pia maeneo yenye mikusanyiko kunapaswa kufungwa vifaa vya kubaini endapo kuna mtu anavuta sigara katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Ofisa Afya wa Soko la Kisutu, Aron Matei aliishukuru TMDA kwa elimu waliyotoa na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kuhusu uvutaji wa sigara katika maeneo yasiyo rasmi.

error: Content is protected !!