Uchambuzi wa kina kuhusu ubora na udhaifu wa Yanga

HomeMichezo

Uchambuzi wa kina kuhusu ubora na udhaifu wa Yanga

Timu ya soka ya Yanga, imekuwa na mwenendo mzuri katika msimu huu. Baada ya kuwafunga wapinzani wao Simba kwenye mchezo wa ngao ya jamii, Yanga imeendelea kutoa kibano kwa kila timu iliyokutana nayo kwenye Ligi Kuu Tanzania.

Click Habari imezungumza na mchambuzi maarufu wa soka nchini, Jemedari Said pamoja na wataalam wengine wa soka nchini ambao wameichambua Yanga na kueleza ubora wao pamoja na udhaifu.

Kwa kuanza na udhaifu, Jemedari ambaye pia amehitimu mafunzo mbalimbali ya ukocha, anasema Yanga ni dhaifu kwenye umaliziaji.

Jemedari amesema hakuna shaka kwamba Fiston Mayele ambaye anaongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga ni mchezaji mzuri, lakini bado hajawa na msaada mkubwa kwa Yanga. Alitolea mfano wa mechi dhidi ya Ruvu Shooting ambapo Mayele alipata nafasi kadhaa lakini hakuweza kuzifumania nyavu, na kuacha viungo wafanye kazi hiyo.

“Mayele anapata nafasi tatu hafungi, Yacouba kabaki na kipa kashindwa kufunga” amesema mdau mmoja wa soka ambaye hakupend akutaja jina lake.

Kwa maoni ya wataalam, kwa kuangalia idadi ya nafasi zinazotengenezwa na Yanga, safu yao inapaswa kuwa na magoli mengi kwa kuwa ubora wa safu ya ushambuliaji unapimwa na idadi ya magoli.

> Jay Z rasmi Instagram

Kwa upande wa upande wa ubora, Jemedari Said ameainisha maeneo yafuatayo kama sababu zinazoipa Yanga ushindi.

Eneo la kwanza ni ubora wa viungo. Ukiachana na Khalid Aucho ambaye anavuma sana kwa sasa, Jemedari Said anasema mchezaji Yannick Bangala Litombo ni mhimili muhimu sana kwa Yanga kwani anacheza soka la kisasa.

Wakati huo pia Yanga inajivunia kuzidi kuimarika kwa Feisal Salum, pamoja na uwepo wa viungo wengine mahiri kama Tonombe Mukoko, Zaawadi Mauya na wengine.

Eneo la pili linalowabeba Yanga ni uzoefu wa wachezaji wao. Jemedari Said na Ibrahim Masoud ‘Maestro’  wanaeleza kwamba Yanga inafaidika sana kupitia uzoefu wa wachezaji wao katika kucheza mechi ngumu.

“Yanga wana beki mzoefu sana upande wa kulia (Djuma Shabani), na wana kipa mwenye uzoefu wa kutosha (Diarra). Lakini pia tusisahau pale katikati wana beki mwenye uzoefu wa kucheza michezo mingi ya Kimataifa akiwa na timu za vijana (Dickson Job). Kuna wachezaji wengi wenye uzoefu wanaisaidia sana Yanga” amesema Jemedari.

Jemedari pia aligusia ubora wa wachezaji kama Jesus Ducapel Moloko ambaye alisema kasi yake inawapa shida mabeki wengi wa upande wa kushoto.

“Mpira ni mchezo wa mbio, Moloko ana mbio na mawazo ya kujua afanye nini. Wanaocheza naye wanajua wapi wamuwekee mpira, na mabeki wengi wa kushoto hawana kasi ya kushindana naye” amesema Jemedari.

Kuhusu Feisal Salum ‘Toto’ ambaye anaimbwa sana na mashabiki wa Yanga, Jemedari amesema mchezaji huyo anawapa faida Yanga kwenye matukio muhimu uwanjani.

Amesema “Uwanjani kuna matukio, tukio muhimu zaidi ni goli. Ukiwa na Feisal unatarajia kwamba wakati wowote anaweza kukupa faida kwenye matukio kwa kufunga kwa mbali au kusababisha goli”

‘Wananchi’ wana jambo lao msimu huu.

error: Content is protected !!