Waziri Makamba azindua kiwanda cha kuzalisha transfoma

HomeKitaifa

Waziri Makamba azindua kiwanda cha kuzalisha transfoma

Waziri wa Nishati, January Makamba amezindua kiwanda cha kuzalisha transfoma cha kampuni ya Elsewedy Electrica Industrial Complex kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huu uliofanyika leo Jumatatu Septemba 12, 2022 Unakuwa ni awamu ya pili ya uzinduzi wa kiwanda hiki cha kuzalisha vifaa vya umeme kilichopo Kisarawe II Kigamboni Dar es salaam.

Awamu ya kwanza ya kiwanda hiki kilihusisha utengenezaji wa nyaya za umeme ilizinduliwa Desemba 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan.

Awamu ya pili ya kiwanda hicho ambayo inahusisha uzalishaji wa transfoma kina uwezo wa kuzalisha trasfoma 2,500 kwa mwaka na kikitarajiwa kutengeneza ajira 1500.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Waziri Makamba amepongeza uwekezaji huo na kueleza Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.

“Ni mafanikio makubwa kuona awamu ya pili ya kiwanda inakuja ikiwa ni miezi sita tu tangu kuanza kwa uzalishaji wa awamu ya kwanza,” amesema

“Hii inaonyesha kiasi gani mmedhamiria kufanya uwekezaji wenye tija. Upande wetu Serikali tutaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara,” amesema Makamba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Elsewedy Electric East Africa, Ibrahim Qamar amesema uzalishaji huo wa transoma 2500 kwa mwaka unaweza kuongezeka kulingana na uhitaji katika soko.

“Uzinduzi wa kiwanda cha transfoma unazidi kufungua milango ya ushirikiano kati ya Tanzania na Misri. Kiwanda hiki kitasaidia kuingiza utalaam huu hapa Tanzania na kuwajengea uwezo watalaam wa hapa nchini,” amesema

“Ahadi yetu ni kwamba tutendelea kuzitafuta na kuziendeleza fursa ambazo zinaunga mkono mpango mkakati wa kuendeleza viwanda nchini Tanzania,” amesema Qamar.

Kiwanda hicho kilichojengwa na kampuni ya wazawa ya Advent Construction Limited kinatarajia pia kupanua uzalishaji wake wa nyaya na transfoma sambamba na kuanzisha uzalishaji wa mita na PVC.

 

error: Content is protected !!