Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini kutenga fedha za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa katika bajeti za huduma za afya ili wagonjwa wanaohitaji rufaa za dharura wasicheleweshwe kwa kudaiwa michango ya mafuta.
Ametoa agizo hilo Jumatatu, Novemba 9, 2026 akizungumza na wananchi wa Iselamagazi, Jimbo la Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga.
“Tusichangishe mafuta kwenye ambulance. Ambulance ipeleke mgonjwa imharakishwe hospitalini. Ambulance sio daladala. Wala manesi wale sio makondakta wa kukusanya michango ya mafuta,” amesema.
Amemwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha magari hayo yanakuwa na mafuta na yako tayari kuhudumia wagonjwa, huku akisisitiza fedha za mafuta zitengwe kwenye bajeti zinazoandaliwa.
“Kama hamkuweka bajeti na sasa hivi mnaandaa bajeti, nataka ambulance zote ziwe ‘standby’ mgonjwa ambaye anatakiwa kunusuriwa maisha yake asiombwe fedha ya mafuta,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi wanaodaiwa michango hiyo kutoa majina yote matatu ya watumishi wanaohusika na kuelekeza watumishi wanaochelewesha huduma kwa uzembe wafukuzwe kazi badala ya kuhamishwa vituo.


