Wasiwasi umeongezeka katika Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya kufuatia ongezeko la matukio ya uvamizi wa makanisa, hasa yale ambayo hayana walinzi.
Usiku wa Ijumaa katika Kanisa la PCEA Karii lililopo Kangai Ward, eneo la Mwea, wezi wamevamia na kuiba vifaa vya kielektroniki vyenye thamani ya takribani Shilingi 500,000 za Kenya [TZS milioni 10.2]. Vifaa vilivyoibwa ni pamoja na mixer, vinanda viwili pamoja na adapta zake, na betri za vipaza sauti.
Mzee wa kanisa hilo, James Kamau, amesema wezi hao pia walivunja sanduku la zaka lakini hawakukuta fedha yoyote ndani.
Tukio hilo ni kufuatia matukio mengine mawili ya uvamizi wa makanisa wiki iliyopita katika eneo la Kirinyaga Central, ambapo Katika Kanisa la ACK Gatuto, wezi waliiba vifaa vya kielektroniki vyenye thamani ya takribani Ksh 500,000.
Tukio lingine ni katika Kanisa la AIPCA St Phillips Giacai ambapo wezi walidaiwa kuvuruga madhabahu, kutumia Sakramenti Takatifu na kunywa divai ya kanisa baada ya kupekua maeneo mbalimbali ya kanisa.
Aidha, Diwani wa Kangai Ward, James Njiru Wambu, amesema pia kulikuwa na jaribio la kuvunja Kanisa Katoliki la Nyaga usiku wa Jumatano, lakini washukiwa hawakufanikiwa kuingia ndani.
Viongozi wa dini wameitaka serikali kuongeza doria za polisi usiku katika maeneo hayo.


