Zijue Faida na hasara msanii kuwa chini ya ‘Record label’

HomeKitaifa

Zijue Faida na hasara msanii kuwa chini ya ‘Record label’

Je, kipi ni bora, kuwa chini ya Record Label au kuwa msanii unayejitegemea kwa kila kitu? Leo utajifunza faida za hasara za kuwa msanii wa muziki chini ya Record label au kuwa msanii binafsi au msanii unayejitegemea.

Msanii wa kujitegemea Vs Msanii aliyesainiwa chini la label Katika soko la muziki wa leo, imekuwa rahisi kwa wasanii kutoa nyimbo halafu zikafanya vizuri bila kuwa chini ya kampuni ya kusimamia
muziki.

Uwepo wa mauzo ya nyimbo za wasanii mtandaoni, masoko yakimtandao (Digital Marketing) na kukuwa kwa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kumerahisisha sana soko la muziki kwa wasanii.

Kwa mfano msanii Chance the Rapper msanii kutoka Marekani aliwahi kushinda tuzo 3 za Grammy bila kuwa chini ya Record Label  yeyote baada ya kuachia mixtape yake ya ‘Coloring Book’.

Zipo faida za kuachia nyimbo ukiwa kama msanii binafsi, ni zipi faida hizo?

1. 100% za umiliki wa kazi zao
Wasanii binafsi kama vile Harmonize hapa Tanzania wanamiliki 100% za kazi zao, kuanzia kwenye mauzo, usambazaji, masoko na kila kitu.

Wasanii binafsi ubunifu wao hauna mipaka kwa kuwa hakuna aliyejuu au chini anaweza kuingilia kazi yake isipokuwa kwa hiari.

Kile kinachopatikana wanapanga wao wagawane na nani, bei gani na kwa muda gani, hii ni tofauti sana na msanii aliyechini ya lebo ya muziki.

2. Uhuru
Wasanii waliohuru hawahitaji ridhaa ya kufanya matangazo, kusafiri, kuwa na urafiki na mtu fulani au kufanya chochote kile. Katika zama hizi za leo, wasanii wasiokuwa chini ya mtu au kampuni wanafaida ya kupata faida kubwa kibiashara kutokana na kile kinachopatikana kutokuwa na mikono mingi.

Hasara zake ni zipi?

1. Bajeti ndogo na Rasili mali kazi
Kwa msanii asiyekuwa chini ya usimamizi anaweza kukwama kimuziki kutokana na kushindwa kumudu gharama za matangazo, usambazaji, kusafiri, mavazi na gharama nyingine.

2. Connections ndogo
Record labels huwa na connections na watu wengi kwenye redio, televisheni, kumbi za starehe na watu wenye ushawishi mkubwa ambao wanaweza kumfanya msanii awe mkubwa kwa haraka. Hii ni tofauti sana na msanii asiyekuwa chini ya uangalizi wa kampuni, inaweza kumsumbua kupata matamasha, matangazo hata nyimbo zake kuchezwa.

3. Muda mchache
Wasanii wasio chini ya uangalizi hukumbwa na tatizo la kutokuwa na muda wa kutosha kutokana na kufanya kila kitu wenyewe. Kuna muda ni muhimu kupata watu watakaokusaidia kwenye kufanya masoko, usambazaji, ubunifu na pia fikra za namna ya kuteka soko la muziki kirahisi. Watu wote hawa inahitaji muda wa kutosha, kufanya kila kitu mwenyewe kunaweza kukukwamisha vibaya.

Faida za kuwa msanii unayesimamiwa

1. Rasilimali kazi na bajeti nzuri
Hapa kuna kila kitu, msanii haitaji kuwaza sana kuhusu studio ya kufanya muziki, nguo za kuvaa, kutengeneza video ya wimbo wake na hata sehemu ya kulala na hela ya kula. Vyote hivi msanii husimamiwa ili aweze kutengeneza kazi nzuri zenye kuleta matokeo mazuri zaidi sokoni.

2. Connection na Network kubwa
Wasanii waliosimamiwa huwa na connection ya kueleweka, ndio mana wakitoa tu wimbo ni rahisi wimbo huo kukua haraka na kusikika sehemu nyingi ndani ya muda mfupi. Watu wanaomiliki hizi labels huwa na ushawishi kwa watu watu ndani hadi nje ya mipaka ya nchi, ni tofauti kwa wasanii ambapo hawana usimamizi.

3. Jina kubwa
Jina la msanii anayesimamiwa linakuwa haraka sana, kwakuwa kazi zake zinafika sehemu nyingi haraka, basi hata utajo wake unakuwa mkubwa kwa watu wingi na kusababisha msanii kupata matangazo na dili nyingi za kutengeneza pesa. Hii ni tofauti sana kwa msanii ambaye hayuko chini ya usimamizi.

Hasara zake ni zipi?

1. Msanii hana umiliki wa kazi zake
Label inaweza kufanya kitu chochote na muziki wako bila ridhaa yako. Kama label imeweza kuwekeza hela zake katika maisha yako, basi hata wao wanaweza kufanya chochote, wakati wowote. Labal ndio inasimamia masoko na usambazaji wa kazi zako, muda mwingine unaweza hata ukadanganywa kiasi halisi cha mapato muziki wako unachoingizia label, na bado msanii akabakia kwenye mabano asijue cha kufanya. Nadhani mmemsikia Harmonize akilalama kuwa siku za mwisho kabla ya kutoka kwenye lebo ya WCB, hakuwa anapewa kiasi chochote kutoka kwenye mapato yanayoingia kupitia mitandao.

2. Mapato hafifu
Record Labels zinachukua asilimia kubwa kwenye mapato yanayoingia kutokana na kazi za msanii. Hapa nazungumzia mapato ya dili za leseni, kama wimbo utatumika kwenye tangazo, filamu, streams, na kila aina ya kazi mziki wa msanii utakayofanya basi ni lazima asilimia ipate asilimia yake. Kweli hii ni biashara kati ya msanii na lebo, lakini haituzuii kusema kubwa mara nyingi wasanii hawapati faida kubwa inayoendana na kazi wanazozifanya, ndio mana mara nyingi mambo haya haya huishia kwenye uhasama mkubwa.

3. Msanii hana hatimiliki
Record label ndiyo inayomiliki haki zote za muziki wa msanii. Licha ya kwamba melodi ni ya msanii, sauti ni ya msanii, ubunifu na mashairi, lakini mwisho wa siku kazi ya sanaa ni ya record label. Msanii Harmonize kulipa milioni 600 WCB ilikuwa ni kununua haki za muziki wake ili aweze kuutumia anavyoweza kwenye matangazo, matamasha na biashara nyingine.

4. Mikataba mibovu
Wasanii wengi wanatoka katika familia za kimasikini, wengine hawana elimu kwenye masuala ya sheria hivyo kuwapelekea kuingia mikataba mibovu kutokana shinikizo linalotokana na njaa zao. Mikataba hii huwabana na kuwafunga baadae wanapotaka kutoka kuendelea kusimamia fedha zao wenyewe.

Hitimisho

Je? utatoka kimuziki ukiwa chini ya usimamizi au kama msanii binafsi, kila moja ina faida na hasara zake. Utakaa chini na kufikiria namna gani utafanya muziki wako, uamuzi ni wako kwani wewe ndio mwamuzi wa mwisho wa maisha na tasnia yako.

error: Content is protected !!