Kundi la nyani wa hifadhi ya Gombe iliyopo kijiji cha Mwamgongo wilayani Kigoma, limevamia nyumba ya Shayima Faya (20) na kumpokonya mtoto mchanga wakati akimnyonyesha na kutokomea naye porini ambapo baadaye mtoto huyo alifariki dunia.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 20, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama amesema tukio hilo limetokea Juni 18, 2022 katika kijiji hicho.
Amesema baada ya tukio hilo mwanamke huyo alipiga kelele kuomba msaada na majirani walijitokeza kumdhibiti mnyama pori huyo ambaye alimtupa mtoto huyo chini akiwa tayari amejeruhiwa kichwani, usoni na mguu wa kushoto.
“Wananchi walifanikiwa kulikimbiza kundi hilo la nyani lililomvamia mwanamke huyo wakati akimnyonyesha wanaye, na kufanikiwa kumpata mtoto akiwa amejeruhiwa lakini baada ya kufikishwa kituo cha afya Mwamgongo alifariki dunia,”amesema Manyama.
Katika tukio jingine watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki na visu walivamia duka la mfanyabiasha Livingston Godluck (35) na kupora Sh5 milioni pamoja na simu za mkononi ambazo bado hadi sasa thamani yake hazijafahamika.
Kamanda Manyama amesema tukio hilo limetokea Juni 19, 2022 eneo la stendi ya zamani kata ya Kibondo wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Amesema katika tukio hilo wanamshikilia mtu mmoja mwenye miaka 25, walimkamata porini akiwa amejeruhiwa na risasi na baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika na tukio hilo na kuwataja wenzake ambao walifanikiwa kutoroka na kurudi nchini Burundi.