Rais Samia Suluhu Hassan ametangazwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Watetezi na Amani kuwa mshindi wa tuzo mbili za kimataifa ikiwemo ya amani duniani 2022.
Tuzo nyingine aliyotangazwa kuwa mshindi ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuipata ni tuzo ya Rais wa Dhahabu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudencia Kabaka amesema Rais Samia alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hizo wiki iliyopita na atakabidhiwa tuzo hiyo Oktoba 24, mwaka huu.
Akizungumza jana Jumamosi Oktoba Mosi, Kabaka amesema miongoni mwa mambo yaliyomfanya Rais Samia kupata tuzo hizo ni uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu ndani ya kipindi kifupi cha uongozi, utetezi wa masuala ya amani ikiwemo uhuru wa kuabudu na amani.
Mengine ni kujali masuala ya kijinsia kwa kuteua wanawake wengi katika uongozi, ujenzi wa madarasa katika shule za sekondari na msingi na utoaji wa elimu bila malipo.
“Sisi UWT na wanawake wote wa Tanzania tumeona fahari sana kwa kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Mheshimiwa Samia. Rais wa kwanza Afrika mwanamke kushinda tuzo mbili na kuandika historia ya kipekee nchini,” amesema.
Maraisi waliowahi kupata tuzo hizo kwa Afrika ambazo Rais Samia atakabidhiwa Oktoba 24, mwaka huu kwa Afrika ni Rais wa Liberia, George Weah na Rais wa Botswana Ian Tseretse Khama.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kupokea tuzo akiwa madarakani baada ya Mei 22, 2022 alipokea tuzo ya Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022 (Babacar Ndiaye Trophy 2022) ikiwa ni kutambua jitihada anazozifanya katika ujenzi wa miundombinu nchini.