Benki ya Standard Chartered imetangaza kufanikisha mpango wa ufadhili wa pamoja wenye thamani ya dola bilioni 2.33 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumanne, fedha hizo zitatumika kujenga sehemu mbili za reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,219, itakayounganisha jiji la kibiashara na bandari ya Dar es Salaam na jiji la Mwanza.
Ujenzi wa mradi huo utatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya Uturuki Yapi Merkezi kwa kushirikiana na kampuni ya China China Civil Engineering Construction Corporation. Ufadhili huo umetokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo mashirika ya mikopo ya mauzo ya nje, benki za kibiashara pamoja na taasisi za fedha za maendeleo.
Standard Chartered imesema kuwa mradi huo wa SGR utachangia kuunganisha bandari ya Dar es Salaam na maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi magharibi mwa Tanzania pamoja na nchi jirani, huku ukitoa njia ya uhakika ya usafiri kwa abiria na usafirishaji wa mizigo.
Aidha, reli hiyo inatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya ndani ya nchi. Tanzania inalenga kujenga mtandao wa reli ya kisasa wenye urefu wa angalau kilomita 2,561, utakaoziunganisha nchi jirani zisizo na bandari kama Rwanda, Burundi, Uganda na Democratic Republic of the Congo.



