Polisi Mkoa wa Arusha wanaendelea kuchunguza mazingira yaliyosababisha kifo cha Sefu Mussa (25) na kujeruhiwa kwa Salimu Haji maarufu Chambega, baada ya wawili hao kufikishwa katika Hospitali ya Lutheran wilayani Karatu, ambapo mmoja alithibitishwa kufariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wawili hao pamoja na mwenzao Abdallah Nuru maarufu Ngandana, walikamatwa na askari wa Uhifadhi wa Ngorongoro Agosti 12, 2026 kwa madai ya kuingia katika eneo la hifadhi kinyume cha utaratibu wakiwa na pikipiki ambazo haziruhusiwi kuingia ndani ya hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, watatu hao walidai kuwa walikuwa wakisafiri kutoka Arusha kuelekea Babati kuhudhuria msiba, lakini walipotea njia na kujikuta wakiingia katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichotokea baada ya kukamatwa kwao hadi kusababisha kifo cha Sefu Mussa, kujeruhiwa kwa Salimu Haji na kurejea salama kwa Abdallah Nuru jijini Arusha.


