Soma hapa ushahidi mpiga picha wa Sabaya kwenye kesi ya kina Mbowe

HomeKitaifa

Soma hapa ushahidi mpiga picha wa Sabaya kwenye kesi ya kina Mbowe

Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu imeendelea leo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu.

Katika kesi hiyo, shahidi wa pili upande wa Jamhuri Justine Eliya Kaaya aaliyeanza kutoa ushahidi leo, aliwahi kuwa mpiga picha wa viongozi mbalimbali akiwemo aliyekuwa mkuu wa Wilya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Katika ushahidi wake Kaaya amesema “Sabaya mara kwanza nilikutana naye 2017 katika uchaguzi mdogo Longido. Wakati huo alikuwa Diwani Kata ya Sambasha, Arumeru na alivutiwa upigaji wangu wa picha. Sabaya alinitaka nikamsaidie kazi hiyo na shughuli nyingine mbalimbali ndani katika kata yake. Nilimkubalia kwa sababu ilikuwa ni fursa kwangu. Nilihama Longido kwenda Arusha, nyumbani kwa Sabaya Kibanda Maziwa, Sakina.

Nilikuwa nikiishi na Sabaya na mkewe na nilifanya naye kazi hadi mwaka 2018 Julai alipoteuliwa kuwa DC Hai, nilikwenda kuishi naye katika makazi ya DC Hai, Kilimanjaro. Hapo nilikuwa msaidizi wake katika shughuli ndogo ndogo Kama kumpelekea nguo zake Dry Cleaner, chai na chakula ofisini kila siku. Hapo niliishi na  Sabaya na mkewe na mwezi Oktoba, 2018 niliamua kurudi Longido kuendelea na majukumu yangu mengine, sababu niliacha mchumba na nilitaka nikasimamie shughuli zangu za kilimo.

Mwezi Novemba 2018 siku moja jioni nikiwa nyumbani nilipigwa simu kwa namba yangu ya airtel 0693006700 na namba ya Airtel 0784779944 na mtu aliyejitambulisha kama Freeman Mbowe. Kwanza nilishtuka kwani sikuwahi kuwasiliana naye.

Aliponipigia aliniuliza hujambo nikamwambia sijambo akasema nina shida ya kukuona ni muhimu sana. Nilimuuliza mahali aliko akanijibu yuko Arusha. Nikamwambia niko Longido na nina changamoto ya usafiri. Aliniambia chukua gari Noah nitakuja kulipa gharama baada ya wewe kufika Arusha.

Lakini, kwa sababu ya ile hofu nilimwambia sitakuja kwanza ni kiongozi mkubwa simfahamu na sina ukaribu wowote na yeye. Aliniambia subiri nakupigia akakata simu na baada ya muda alinipigia tena akaniambia niko njiani nakufuata Longido.

Kwa sababu alishaniambia yuko njiani anakuja nilishindwa kumzuia nikasema acha nimsubiri nisikie anachotaka kuniambia. Baada ya dakika 40 alinipigia tena simu akaniambia njoo hapa uwanja wa mpira Longido. Nilimuita bodaboda anipeleke pale, nikakuta gari liko pale linaunguruma na muda huo ilikuwa ni saa 3 usiku.

Nikimpigia simu kwenye namba ileile  ya 0784779944, akaniambia sogea kwenye gari. Nikasogea akashusha kioo cha dirisha akaniambia ingia kwenye gari chief usiwe na wasiwasi. Nikamruhusu yule  boda akaondoka nami nikafungua gari mlango wa nyuma nikaingia.

Alikuwemo yeye na upande wa dereva alikuwepo mwanamke. Aliniambia kwamba Lengai anasumbua sana pale Hai na mimi ni mtu wake wa karibu. Akawa anataka nimpe taarifa ya shughuli anazofanya na watu  ambao yuko nao pale Hai. Nikamwambia haitawezekana kwa sababu mimi sipo tena na Sabaya.

Aliambia yeye ni kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani kwenye nchi hii, hivyo atafanya namna yoyote atakayoweza nirudi kwa Sabaya niendelee na kazi. Nilimwambia haitawezekana sababu nimechagua kufanya kazi zangu binafsi.

Aliniambia samahani kwa kukusumbua na alinipa Sh300,000, nikamuuliza ni za nini akaniambia ni za usumbufu tutawasiliana. Tuliagana akaondoka

Niliposhuka kwenye gari nikampigia Lengai simu nimpe taarifa, lakini hakupokea simu. Niliendelea kusimama pale uwanjani na baadaye nilimpigia mbunge wa Longido, Dk Steven Kiruswa kumweleza habari hizo. Nilimuita boda boda nikarudi nyumbani.

Mwanzoni mwa mwaka 2020, alinipigia tena simu kwa mtandao wa WhatsApp kwa namba ileile baada ya salamu aliniambia tumepotezana sana Chief, aliniambia anataka tuonane, nimfuate Moshi wakati huo mimi nilikuwa Arusha. Nilimwambia niko shambani kumwagilia nikishamaliza nitakuja.

Baada ya shughuli zangu nilipanda Coaster nikampigia simu kumpa taarifa kwamba ninakwenda. Baada ya kumpa taarifa aliniambia nishuke Machame Road, Wilaya ya Moshi mkoni Kilimanjaro.

Baada ya kufika nilishuka kwenye gari na kumpigia simu kwa namba yake ileile ya Airtel. Aliniambia nisubiri hapo anakuja.

Baada ya muda akanipigia simu akaniambia nimefika umekaa upande upi nikamwambia nimekaa upande wa kushoto  akaniambia njoo upande wa kulia. Kuna njia ya Machame na nyingine ya Arusha.

Nilipofika nikakuta gari V8 nyeusi yenye mlingoti na bendera ya Bunge yenye plate number za KUB. Ilisimama karibu yangu ikashusha kioo cha upande wa abiria na hapo nikamuona mwenyekiti Freeman Mbowe akaniambia panda. Alishuka mtu kutoka kwenye kiti cha abiria nyuma akaniambia pita.

Tuliendelea kuzungumza ile gari ilichukua uelekeo wa Machame, baada ya dakika kama nane iliingia mahali ni Hotel ya Aishi.

Ndani ya gari kulikuwa na dereva na huyo mlinzi wake aliyenipisha nikaingia kwenye gari. Nilikuwa sifahamiani nao. Aliyenipisha nilijua ni mlinzi wake baada ya kunitambulisha kuwa ni mlinzi wake Kanda ya Kaskazini na pia ni Diwani wa Kata ya Kibororoni.

Ile hotel nilitambua kwa sababu niliona kibao kilichoandikwa Aishi Hotel.

Baada ya kushuka kwenye gari mimi, Mbowe na yule mlinzi wake, tulienda kuketi upande wa mgahawa, akaniambia kuwa tutazungumza kwa muda mfupi kwa sababu ana mikutano ndani ya jimbo.Aliniambia niagize kinywaji au chakula. Muda huo ilikuwa saa 7 mchana na simu ya kunitaka tukutane alinipigia saa 2:30 asubuhi.

Safari ya kuelekea Moshi kutoka Arusha niliianza saa 5 kasoro asubuhi na nilianzia sehemu inaitwa Kilala wilayani Arumeru.

Kwanza Mbowe aliuliza “kuna mipango gani juu ya hii mikutano ninayoifanya jimboni?” nikamwambia sijui chochote kinachoendelea. Aliniambia nimtajie majina ya wasaidizi wa Sabaya anaotembea nao, nilimwambia sina taarifa yoyote ya kumweleza. Nilimtajia yale majina na yule Diwani akawa anayaandika kwenye karatasi, majina ya Japhet Lwendela, Vedastus Sigula, Mtoto wa Mkulima, Sylvester Nyegu, Binti wa Kichaha, mwalimu Doreen na Watson Malimungu.

Akataka na namba zao za simu, nikazitaja wakaziandika akasema atashughulika nao tutawasiliana mimi na yeye baadaye.

Baada ya mazungumzo Freeman Mbowe aliniaga kuwa anakwenda kwenye mikutano na kwamba, baadaye atanitumia chochote kwenye simu yaani nauli. Alitimiza ile ahadi lakini hakunitafuta baada ya pale. Baada ya pale nilirudi Arusha.

Mwezi wa 7 2020, Siikumbuki tarehe alinipigia kwa namba yake ya Airtel kwa njia ya mtandao wa WhatsApp namba ya 0784779944, aliniambia niko njiani natoka Dar naomba jioni tuonae nina jambo la muhimu kuzungumza na wewe uje Moshi. Wakati huo nilikuwa shambani kwangu na ilikuwa mchana saa 8.

Niliendelea kufanya shughuli zangu ilipofika saa 11 jioni nilianza safari ya kwenda Moshi, nilipanda basi la Kiumbocharo liliokuwa likitoka Singida. Aliniambia kuanzia saa 1 usiku atakuwa amefika Moshi. Nilishuka Moshi stendi saa 1:30 usiku.

Nilimpigia simu namba yake ileile nikamwambia nimefika., aliniambia nichukue pikipiki nimfuate Kizo hotel mjini Moshi.

Nilichukua bodaboda nikamwambia nipeleke Kizo hotel nilipofika nikampigia Mbowe simu  0784779944 nikamwambia nimefika. Aliniambia namtuma msaidizi wangu akufuate. Baada ya muda alikuja dereva wake ambaye namkumbuka kwa jina moja la Willy, sababu tulipokutana mara ya kwanza Machame ndiye  alikuwa anamwendesha.

Tulikwenda nyuma ya hotel ambako kuna swimming. (Willy) aliniambia Mheshimiwa yuko kwenye kikao, hivyo tukae hapa tumsubiri amalizie kikao.

Japo tulikuwa na mlinzi wake ambaye alikuwa baunsa kidogo, ambaye Willy aliniambia kuwa nisiwe na wasiwasi. Tulikula yule mlinzi wake alielekea alikokuwa Mbowe baada ya muda mfupi alirudi akasema tunaondoka.

Aliniambia (Freeman Mbowe) pole sana kwa kukuweka, yule mlinzi wake alinifungulia mlango wa gari na yeye mwenyekiti aliingia na nyuma aliingia aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Joyce Mukya nikakaa katikati na upande wa nyuma, Mbowe akakaa mlinzi wake.

Baada ya pale kutoka Kizo hotel gari ilielekea uelekeo wa Arusha mpaka Aishi Hotel Machame.

Baada ya kushuka kwenye gari akamwambia yule mbunge atangulie ndani sisi tuna kikao kifupi.

Tulikaa upande wa mgahawa, Mbowe, mlinzi wake, dereva alipotaka kujumuika akimwambia hiki kikao ni cha watu watatu wewe kaa pembeni hakikuhusu.

Alinitambulisha akiniambia yule ni mlinzi wake na msiri wake anaitwa Halfan Bwire hivyo niwe huru kujumuika naye.

Huyo mlinzi tulikuwa tumekaa naye mkono wake wa kushoto.

Aliniambia nimtajie tena majina ya wale wote watu wa Sabaya na namba zao za simu na kazi wanazozifanya kwa Sabaya. Kabla sijaanza kumtaja alimwambia mlinzi wake yule Halfani Bwire achukue kalamu na karatasi ili aandike. Baada ya kurudi aliniambia nimwandikie. Hivyo nilianza kuandika majina na namba za simu.

Wale walikuwa ni marafiki zake na Sabaya ambao nilikuwa nawafahamu na namba zao za simu nilikuwa nazo kwenye simu maana tulikuwa tunafahamiana.

Majina aliyoandika ni yale ya mwanzo nyongeza ni Enock Kirigiti.

Baadaye alinitaka nimtajie mahali Sabaya anapenda kutembelea, nilimtajia.

Baada ya kutoa taarifa hizo nikimuuliza Mwenyekiti hizi simu unataka za nini? Akaniambia hilo niachie mimi kazi yako hapa imeisha.

Baada ya pale aliniambia nimkabidhi Halfani Bwire yale majina,  Halfani Bwire akasema huyu Sabaya ni mtu mdogo sana nitamchezesha.

Baada ya pale mwenyekiti aliniambia kazi imeanza rasmi kuanzia sasa hivi nitakuwa nakulipa mshahara.

Muda huo ilikuwa ni saa 4 usiku.

Baada ya pale alisema utapewa chumba ulale hapa utaondoka asubuhi . Sababu sikuweza kupata usafiri kwenda Arusha ikibidi nilale pale. Asubuhi Ile alinitumia Sh200,000 kwa 0754916666 kutoka namba yake ya Airtel, airtelmoney 0784779944.

Kulipokucha nilirudi  Arusha saa 12 asubuhi kuendelea na shughuli zangu za shambani

Hatukuweza kuonana tena kwa sababu Agosti 25 2020 nilikamatwa na Jeshi la Polisi.

Nilikamatwa Makumira wilaya ya Arumeru nikiwa naenda benki ya CRDB kupeleka hela.

Nilikuwa napeleka Fedha baada ya kuuza mazao ya shambani karoti ambayo nilikuwa nimewauzia watu wa Mount Meru. Nilikuwa na Sh1,117,000 Dola 1,100 za Marekani naEuro 240

Niipokamatwa nilipelekwa kituo kikuu cha Arusha na baada ya saa moja nikienda kupekuliwa nyumbani kwangu kisha nilisafirishwa kuletwa Dar.”

Kaaya amesema baada ya kuletwa Dar es Salaam alifikishwa katika Kituo Kikuu cah Polisi,na baadae alifikishwa Mahakamani na kuunganishwa na Mbowe na wenzake watatu katika kesi ya ugaidi, lakini baada ya upepelezi kukamilika yeye alifutiwa mashtaka.

error: Content is protected !!