Mganga mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe ametoa taarifa kuhusu maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa UVIKO-19 na kusema kwamba mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kuongoza kwa kuwa na wagonjwa wapya 184 kati visa vipya 252 vilivyoripotiwa.
Kwa kipindi cha Januari 29 hadi Februari 6, mwaka huu ndio muda ambao visa hivyo vimeripotiwa huku wagonjwa wapya 76 kati ya 78 waliolazwa wakiwa ni wale ambao hawajachanjwa na vifo vilikuwa vitatu.
“Tangu ugonjwa huu ulivyoripotiwa kwa mara ya kwanza hapa nchini mnamo Machi 2020 hadi kufikia Februari 6, mwaka huu, jumla ya watu 33,482 walithibitika sawa na asilimia 7.6 kati ya 442,566 waliopima na jumla ya watu 792 wapepoteza maisha,” alibainisha Mganga Mkuu, Aifello Sichalwe.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendelea kuchukua thadhari za kujikinga na ugonjwa huo ikiwamo kuchanja chanjo ya UVIKO-19, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa kwa usahihi, kuzingatia usafi binafsi kwa kunawa mikono, kuwahi kwenye vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa huo na kuzingatia kufanya mazoezi.