Fahamu makao makuu ya kuku Tanzania

HomeKitaifa

Fahamu makao makuu ya kuku Tanzania

Ni rasmi sasa Mkoa wa Tabora ndiyo unaoongoza kwa kuzalisha kuku wengi zaidi wa kienyeji Tanzania baada ya takwimu mpya kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kubainisha kuwa mkoa huo una zaidi ya kuku hao milioni 2.82 ukiupita Mbeya ndani ya miaka miwili iliyopita.

Ripoti ya Mwaka ya Sekta ya Kilimo ya Mwaka 2016/17 (Annual Agricultural Sample Survey Crop and Livestock 2016/17) iliyotolewa hivi karibuni na NBS inaonyesha kuwa Tabora ilikuwa na kuku wa kienyeji 400,000 zaidi ya wale waliokuwepo mwaka 2014/15 jambo linaloufungua mkoa huo na fursa lukuki za biashara zitakanazo na kuku.Tabora una asilimia 7.3 ya kuku wote wa kienyeji nchini. Hii ina maana kuwa kuku saba kwa 100 waliopo nchini wanazalishwa Tabora.

Katika utafiti wa NBS wa mwaka 2014/15, Tabora ilikuwa ya pili baada ya kuzalisha kuku wa kienyeji milioni 2.4 ukiwa nyuma ya Mbeya uliokuwa umeongoza kwa kuwa na ndege hao milioni 2.5.

Mkoa Singida ambao baadhi ya wananchi hudhani ndio unaongoza kwa uzalishaji wa kuku wa kienyeji hapa nchini kwa miaka mingi, safari hii umebahatika kuingia katika nafasi ya tatu kwa kuwa na kuku zaidi ya milioni 2.1 baada ya kuwa nje ya orodha ya 10 bora katika utafiti uliopita wa AASS mwaka 2014/15. Singida wenye asilimia 5.7 ya kuku wote wa kienyeji nchini  upo nyuma ya mkoa wa Shinyanga.

Mbeya ambao ulikuwa wa kwanza katika ufugaji wa kuku wa kienyeji katika utafiti wa mwaka 2014/15 umetupwa hadi nafasi ya tisa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya NBS, kwa ujumla uzalishaji wa kuku wa kienyeji nchini umepanda kwa asilimia 5.7 hadi kufikia kuku milioni 40.34 kutoka kuku milioni 38 mwaka 2014/15. Kati ya kuku hao waliopo nchini kwa sasa, ni asilimia nne tu au kuku wanne kwa kila 100 wanazalishwa visiwani Zanzibar.

Mikoa hiyo 10 kwa pamoja inazalisha takribana nusu ya kuku wote wa kienyeji hapa nchini ukilinganisha na mikoa 20 iliyosalia.

Kati ya mikoa hiyo 10 inayoongoza kwa kuzalisha kuku wengi, mitano inatoka Kanda ya Ziwa ambayo ni Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza. Mikoa hiyo kwa pamoja inazalisha kuku zaidi ya milioni 10.9 huku mikoa mitano iliyobaki ya Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa na Singida kwa pamoja ikizalisha kuku wapatao milioni 9.6.

NBS inasema ripoti hiyo ina lengo la kutoa ufahamu mpya kwa ajili ya mipango ya watunga sera, watafiti na watu wengine wanaohusika katika sekta ya kilimo ili kuboresha mazingira yaliyomo kupitia takwimu sahihi, muhimu na za kuaminika katika kilimo ili kuamua ukuaji wa kisekta, kupima ajira na kupunguza umaskini.

Pamoja na baadhi ya mikoa Tanzania kuzalisha kuku wa kienyeji kwa wingi bado sehemu kubwa ya wafugaji wanafuga kwa kutumia mbinu za kienyeji jambo linalofanya wapate mavuno kidogo na yasiyo na faida ya kutosha tofauti na ambavyo wangefuga kisasa.

source: Nukta

error: Content is protected !!