Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tamasha la Kizimkazi limekuwa sehemu muhimu ya safari ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Kusini, maeneo jirani na Zanzibar kwa ujumla.
Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, wakati akizungumza katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi, ambapo ameeleza kuwa kila mwaka tamasha hilo linapoandaliwa huacha alama katika maendeleo ya eneo hilo.
Amesema tofauti na mwaka 2016 wakati tamasha hilo lilipoanza, Kizimkazi imeendelea kuwa na fursa nyingi za biashara na uwekezaji kutokana na ujenzi wa miundombinu na miradi mbalimbali inayovutia wananchi na wawekezaji.
“Tunawakaribisha kuja kuwekeza, mazingira mazuri ya uwekezaji yamekwishawekwa,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaendelea kujenga uwanja wa michezo ambao ukikamilika utatumika katika michuano ya AFCON 2027, huku akiwataka wawekezaji kutumia fursa hiyo kuwekeza katika huduma zitakazohitajika kwa wachezaji na washiriki wa michuano hiyo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka Watanzania kuendelea kuzitunza tunu za amani na utulivu, akisisitiza kuwa maendeleo, uwekezaji, biashara, utalii, ajira na huduma za jamii haviwezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani.


