Lindi washukuru fedha za tozo kwa kuboresha sekta ya Afya

HomeKitaifa

Lindi washukuru fedha za tozo kwa kuboresha sekta ya Afya

Wakazi wa kata ya Mvuleni, manispaa ya Lindi wameeleza watakavyonufaika na uwepo wa kituo cha afya cha kisasa kilichojengwa kutokana fedha za tozo za miamala ya simu kikiwa na thamani ya Sh250 milioni.

Wananchi walieleza hayo jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumzia umuhimu wa kituo cha afya cha Mvuleni ambacho kipo katika hatua ya mwisho kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa vijiji vitano vya kata hiyo.

Kabla kituo hicho hakijajengwa wananchi walilazimika kwenda kufuata huduma za afya katika kijiji cha Kitomanga wakitembea umbali wa zaidi ya saa moja au zaidi na wakati mwingine walilazimika kwenda mjini umbali wa kilomita 65.

Mkazi wa Mvuleni – Mashariki, Hadija Nampamba alimshuruku Rais Samia kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo, akisema hapo awali walikuwa wakihitaji huduma iliwalazimu kupitia changamoto mbalimbali ili kufanikisha matibabu.

“Zamani mtu akipata ujauzito wanafunga matenga kwenye baiskeli au pikipiki wakupeleke katika hospitali ya Sokoine iliyopo Lindi mjini. Wakati mwingine kina mama wanajikuta wanajifungulia njiani kutokana na umbali wa hospitali au kupoteza maisha na mtoto.

“Hii ilikuwa adha kubwa kwa kina mama lakini tunaishukuru Serikali yetu kwa kutujali na kutusogezea huduma hii. Sasa hivi zile adha za kuelekea zahanati ya Kitomanga au Lindi Mjini zitapungua, hiki kituo kipo karibu na unatembea muda mchache sana,” alisema Hadija.

Hadija alitolea mfano miaka ya nyuma mdogo wake mjamzito aliposhikwa na uchungu, walimuweka kwenye tenga na kupakiwa kwenye pikipiki kumsafirisha hadi Lindi mjini ambako hata hivyo, ndugu yake huyo pamoja na mtoto walifariki dunia.

Mkazi wa Kijiji cha Maloo kichopo ndani ya kata Mvuleni, Kazibure Abdallah aliishuruku Serikali kwa ujenzi wa kituo cha afya, akisema kikianza kutoa huduma kitaupunguzia umbali wa kutembea hadi kijiji cha Kitomanga ambapo gharama yake Sh 10,000.

“Sasa hatutakwenda Kitomanga maana kulikuwa mbali na gharama yake kubwa, wakati baadhi yetu uwezo mdogo.Kikianza kufanya kazi tutakuwa tunalipia gharama ya Shilingi 3000,” alisema Kazibure.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele alisema walipokea Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Mvuleni na Nga’pa ambayo vipo hatua ya mwisho kukamilika kwake.Alisema kutoka kituo cha afya za Mvuleni hadi Lindi Mjini ni kilomita 65

“Huduma za afya zikianza kutolewa matarajio yetu kina mama wajawazito na watoto watapata matibabu hapa tena kwa wakati.Kwa hatua hii tutapunguza vifo vya kina mama na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano,” alisema Mnwele.

Hata hivyo, juzi Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) anayeshughulikia afya, Dk Grace Maghembe vituo vya afya vilivyokamilisha majengo ya awali kupitia fedha za tozo, vitapewa fedha zingine kwa ajili ya kuongeza majengo matatu.

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainab Telack alisema vituo vya afya nane vilivyojengwa katika mkoa huo, vimezingatia mahitaji mahsusi, akitolea mfano cha Mvuleni,akisema kikianza kutoa huduma kitawanufaisha wananchi wa vijiji vitano waliokuwa wakipata changamoto.

error: Content is protected !!