Njia za kujikinga na kupasuka midomo na ngozi kukauka

HomeElimu

Njia za kujikinga na kupasuka midomo na ngozi kukauka

Ni kawaida kila ifikapo mwezi Juni hadi Agosti kila mwaka, maeneo mengi nchini Tanzania kuwa na hali ya baridi na upepo. 

Hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk  Ladislaus Chang’a alisema kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), huwa ni kipindi cha baridi na upepo kwa maeneo mengi ya nchi. 

“Katika kipindi cha JJA, 2022 hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki,” alisema Dk Chang’a.

Alisema kutokana na kubadilika kwa mifumo ya hali ya hewa hasa baharini, vipindi vya upepo vinaweza kutokea hasa kwa wakazi wa mikoa ya pwani. 

Hali hiyo husababisha athari mbalimbali za kiafya kwa watu ikiwemo baadhi kupata michubuko kwenye mdomo, pua na sehemu nyingine za mwili. Wengine ngozi zao huwa kavu na kuwapotezea mwonekano wao wa awali. 

ukiwa ni miongoni mwa watu ambao wamepata changamoto hizo za kiafya, usihofu kwa sababu suluhisho lipo.

Hatua za kujikinga na kupasuka midomo na ngozi kukauka

Paka mafuta mengi kwenye ngozi

Dk Sultan anasema ili ngozi isiwe kavu, inatakiwa watu waongeze unyevunyevu kwenye ngozi kwa kupaka mafuta.

“Katika kipindi hiki ni vyema sana kupaka mafuta kwa wingi. Mafuta yawe ya kawaida mfano ya nazi, sishauri mtu atumie losheni kwani  losheni inachochea ukavu,” amesema Dk Sultan.

Tumia mafuta ya kujilinda na mionzi ya jua (sunscreens)

Baadhi ya watu wana ngozi nyepesi ambazo huathirika sana na mionzi ya jua. Katika kipindi hiki watu wa aina hiyo wanatakiwa kutumia mafuta ya kujilinda na mionzi hiyo kwa kiasi kikubwa.

“Paka mafuta ya kukulinda na mionzi ya jua, ili kutunza unyevu nyevu unapokua juani au kwenye mwanga mkali. Hii itakulinda na madhara zaidi yatakayotokea katika kipindi hiki cha hali ya ubaridi,”ameomgeza Dk Sultan.

Tumia muda mchache wakati wa kuoga

Kipindi hiki cha baridi watu hupenda kuoga maji ya mojo, Dk Sultan  anashauri mtu akioga maji ya moto atumie muda mfupi, kwa sababu maji ya moto na yenyewe ni chanzo cha kukausha ngozi.

“Mtu anapooga haifai uchukue muda mrefu, uoge maji ya moto lakini kwa muda mfupi ili usipoteze unyevu wa ngozi yako wakati unaoga,” amesema mtaalam huyo wa afya ya binadamu.

Kupaka mafuta kabla ya kuvaa nguo ndefu na kujifunika

Kwa kipindi cha baridi ni kawaida watu kujifunika nguo nzito ili kujikinga na baridi, anashauri mtu ajifunike wakati mwili ukiwa na unyevu wa kutosha.

“Ni vyema mtu akijifunika awe amepaka mafuta ili kuupa mwili unyevu unaotakiwa, ukijifunika ukiwa hujapaka mafuta unachochea ngozi kupata cracks (michubuko),” amesisitiza mtaalamu huyo.

Hata hivyo, ngozi kukauka au kupasuka kwa midmo ni suala la kawaida ambalo hutokea nyakati za baridi.

 

SOURCE: NUKTA HABARI

 

error: Content is protected !!