Profesa Mkenda aruhusu vitabu vya ziada

HomeKitaifa

Profesa Mkenda aruhusu vitabu vya ziada

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amepiga marufuku maofisa elimu kuzuia vitabu vya ziada kutumika na kuonya atakayebainika kufanya hivyo hatakuwa na huruma naye na kuitaka Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) kuja na njia mwafaka ya kukabiliana na upungufu wa vitabu vya kiada na kuhakikisha vinapatikana kwa bei nafuu kwa kuwashirikisha wachapishaji wa ndani.

“Tumesema kitabu kiongozi cha kufundishia ambacho ni kiada kitatolewa na TET, lakini vitabu vya ziada vyenye ithibati lazima navyo viwapo ili mwanafunzi aweze kutafuta maarifa zaidi huku na huku na wazazi wapewe orodha ya vitabu vya kiada na vya ziada vyenye ithibati ili kuwa na hiyari ya kununua,”

“Sitomuelewa ofisa ambaye atazuia wanafunzi kusoma vitabu mbalimbali hasa tukizingatia kuwa tunataka kuongeza ari ya usomaji vitabu na upatikanaji wa vitabu. Wanaofanya hivyo waache mara moja, kama kuna ofisa anakwenda mpaka kukagua begi la mwanafunzi ili asiwe na kitabu kingine huyo tukipata taarifa zake hatutakuwa na huruma naye,” alisema Profesa Mkenda.

Aidha, Profesa Mkenda alimuagiza Mkurugenzi wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Dk Lyyabwene Mtahabwa kuunda timu ndogo itakayojumuisha Chama cha Wachapishaji na Chama cha Wauza Vitabu ili kuangalia namna ya kuzishughulikia kwa pamoja hoja zilizoibuka.

 

error: Content is protected !!