Rais Samia: MV Liemba kuchochea uchumi Ziwa Tanganyika

HomeKitaifa

Rais Samia: MV Liemba kuchochea uchumi Ziwa Tanganyika

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za usafiri katika Ziwa Tanganyika, ikiwemo kuimarisha meli ya MV Liemba, ili kuongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji wa mizigo pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na maeneo jirani.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma, Rais Samia amesema maboresho ya MV Liemba ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuunganisha miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa majini ili kurahisisha biashara na mawasiliano ndani ya nchi na nchi jirani zinazotumia Ziwa Tanganyika.

Amesema kukamilika kwa mradi wa SGR pamoja na kuimarishwa kwa huduma za MV Liemba kutafungua fursa mpya za biashara, utalii na uwekezaji, huku kupunguza gharama za usafirishaji wa watu na mizigo katika ukanda huo.

Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuifanya Kigoma kuwa lango muhimu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, hatua itakayoongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi.

error: Content is protected !!