Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Watanzania wanapaswa kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjao uliopo nchini Kenya na kuahidi kuboresha utoaji wa vyeti vya kieletroniki vya homa hiyo mipakani ili kuzuia udanganyifu unaoweza kufanywa na maofisa ili kuwapa vyeti watu wasiopata chanjo.
“Ugonjwa upo kilomita 285 kaskazini mwa Nairobi, ugonjwa uko karibu tudhibiti mipaka yetu kama mtu hana kadi ya chanjo asiruhusiwe kuingia nchini ili kuokoa maisha ya wananchi,” alisema Ummy.
Waziri Ummy alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na homa, kuumwa n akichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika na mwili kuwa na manjano.
Aidha, alisema dalili nyingine ni kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni na wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi.