Upanuzi wa Uwanja wa Ndege Iringa mbioni kuanza

HomeKitaifa

Upanuzi wa Uwanja wa Ndege Iringa mbioni kuanza

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi kwenye upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa utakao rahisisha shughuli za utalii hasa kwa wageni wanaokwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na vivutio vingine.

Pia, uwanja huo utaongeza kasi ya ukuaji wa biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu kusini hususan kutokana na uzalishaji wa mazao mengi kama parachichi, chai na mazao ya miti.

Akiweka jiwe la msingi kwenye uwanja huo leo Ijumaa, Agosti 12, 2022, Rais Samia amesema ujenzi wa uwanja huo ni nafasi ya kipekee kwa wakazi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazofunguliwa.

“Uwanja huu wa Iringa sasa utaanza kupokea ndege kubwa zinazoweza kubeba abiria kuanzia 70 kwenda mbele,” amesema Rais Samia.

Amesema kwa sababu Iringa ni wazalishaji wazuri wa mazao kama parachichi, mbao na chai, uwanja huo utasaidia kusafirisha mazao hayo kwenda nje ya nchi.

“Iringa kuna mradi wa kituo cha utalii ambao hatuja kiendeleza, kwa maana hiyo uchumi wa Iringa sasa unafunguka,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema ujenzi wa uwanja huo unatokana na fedha za Serikali na mkopo wa Benki ya Dunia.

“Ombi langu kwenu  ni kuchapa kazi, anayelima alime kwa wingi, anayefanya kazi za misitu afanye kwa kiwango cha biashara na anayefanya lolote lile afanye kibiasha kwa lengo la kukuza uchumi wa mkoa,” amesema Rais Samia.

Amewataka wakazi wa mkoa huo kujenga tabia ya kulinga miradi ili iweze kuchangia uchumi wa mkoa huo kwa kiasi kikubwa.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Rogatus Mativila alisema kiwanja cha ndege cha Nduli kilianza kutumika mwaka 1950 huku miundombinu yake ilijengwa kati ya mwaka 1970 hadi 1980.

Amesema kiwanja hicho kinachojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh 63.7 bilioni kitakuwa kikihudumia wageni wa ndani ya nchi na watalii wanaokwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Kiwanja cha Ndege cha Iringa ni miongoni mwa viwanja vya ndege 11 nchini vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu kwa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kati ya mwaka 2014 hadi 2017,” amesema.

Amesema awamu ya kwanza ya ukarabati huo inahusisha ujenzi wa barabara za kutua na kutukia ndege.

Mhandisi Mativila amesema katika kiwanja cha Iringa kutakuwa na ukarabati wa barabara ya  kutua na kurukia ndege, maegesho ya ndege, kituo cha huduma za zimamoto na ununuzi wa gari, ujenzi wa kituo cha umeme, uzio wa usalama, mifereji ya maji ya kuondoa maji na jengo la muda la kuongozea ndege.

Leo mchana, Rais Samia atahutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Samora.

error: Content is protected !!